PURUKUSHANI YA MAMA NZIGHE


Kama ilivyo kawaida kila Jumapili jioni, sote wajukuu tulijumuika chini ya mvule na kumngojea babu awasili ili atuhadithie visa vilivyotukia wakati alipokua barobaro. Hadithi za babu zilituburudisha na kutumakinisha vilivyo, hata kuliko elimu tuliyopewa ya darasani kwenye daftari. Mzee huyu mwenye mvi nyeupi pepepe alikua maktaba ya uhalisia.  Nyingi ya hadithi za babu zilikolea ukweli mtupu, ingawa kuna nyakati ambapo alitupaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Hatukujali hayo, kwani hekaya zake zote  zilijaa hekima sufufu.
Leo hii babu alikua atueleze jinsi alifanikiwa kuhama kutoka mtaa wa Madongoporomoka alipokulia na hata kununua shamba Milimani. Ilisemekana kwamba alipokuwa mchanga, akina babu walikua maskini kisonoko bin madiwaba. Ikakuwaje tena alifanikiwa kuipanda ngazi ya maisha akastarehe kati ya mabwenyenye?
Wajukuu na vitukuu wote waliporundikana babu aliwasili huku akijikongoja kama mwenye maradhi ya kifua. Lakini tabasamu lililobandikika usoni mwake lilitudhihirishia kua alikua buheri wa afya. Aliketi kitako, akailaza bakora yake, kisha akasafisha koo.
“Leo nataka niwahadithie kisa cha ghulamu mmoja aliyejulikana kama Nzighe na mamake,” Alianza kusimulia.  Sote tulitulia tuli kama maji ya mtungi na kumuazima masikio yetu.
“Miaka mingi iliyopita, palitokea Kijana huyu Nzighe aliyeishi katika mtaa wa mabanda, Madongoporomoka. Maishani mwake, Nzighe hakuwahi pata bahati ya kumjua babake. Waliishi kwa ufukara uliosononesha na mamake Rodah aliyemlea bila kinyongo na kumpenda kwa dhati.
Kwa akina Nzighe hakukua pahali pa kutamaniwa hata! Hii ni kwa sababu maisha yao yalikua picha halisi ya umaskini unaonuka. Mtoto huyu alikua hohe hahe bin taaban, kwani alikula chakula cha nguruwe na kuenda nusu uchi.
Mamake, japo mwenye umri wa makamo, alionekana kama ajuza kwa vile maisha yalivyomtenda. Alifanya kazi mchana kutwa na usiku badala ya kulala, alitafuta vibarua na kukesha takriban usiku kucha. Mahitaji nayo yalikua mengi, yakamkamua jasho na kumuacha mkavu kama ukuni.
Nzighe alifahamu kwamba ni masomo pekee ambayo yangemkomboa kutokana na uvundo huu wa maisha. Ingawa sare yake ya shule ilikua duni na mbovu iliyoruhusu matako kua nje, alitia fora masomoni huku akijikumbusha kwamba mchumia juani hulia kivulini siku wahed. Alikiheshimu kitabu kama baba na kukithamini kama mama.
Maulana alimwonekania Nzighe na mitihani ilipowasili, alipasi kwa alama za juu akawapiku wanafunzi wote wa Madongoporomoka. Ikathibitika kwa kila adinasi kuwa chanda chema huvikwa pete alipopewa nafasi ya kusomea ughaibuni na shirika moja lisilo la kiserikali. Shirika hilo liliagiza kugharimia masomo yake ya chuo kikuu na hata kuahidi kumtafutia gange pindi tu atakapomaliza masomo. Ama kweli, mgaagaa na upwa hali wali mkavu.
Alipokuwa akifunganya virago, mamake Nzighe alimpa nasaha na kumsihi awe akimtumia pesa mara kwa mara. Wote walifahamu kuwa safari hii ya ng’ambo ndiyo nasafi pekee ambayo ingewaondoa kutoka kundi la malofa na kuwaeka katika orodha ya matajiri.
Maisha kule Ulaya hayakua rahisi jinsi Nzighe alivyokusudia. Kuna nyakati ambapo theluji ingeikoloni ardhi na mara kwa mara angeshindwa kustahimili baridi kali. Lakini alijipa moyo na kumeza mrututu, akajikaza kisabuni hadi akafuzu mitihani yake. Pesa  nazo ziliota mbawa na kuwa adimu kama mayai ya fahali. Alitamani kumtumia mamake hela lakini hakua hata na pesa za kusagia mkungu. Kile alichoweza tu kufanya ni kumtumia mamake mikate ya kule Ulaya.
Siku zikatunga wiki, wiki zikazaa miezi, na miezi ikajirundika miaka. Hatimaye, kijana huyo alimaliza shule na kwa vile alikua na mdahala mzuri na wazungu, akapata kazi kwa mojawapo ya kampuni za mikate kama meneja.
Lakini tabia yake ya kumtumia mamake mikate haikufikia kikomo. Alizidi kuituma mikate nyumbani Madongoporomoka wiki nenda wiki rudi. Mamake alidhani mwanaye ameingiwa na mghafla, kwa kua alimueleza atume pesa naye akatuma mikate.
Tabia hii ya kutuma mikate ikaanza kumla mamake roho. Alianza kuguna, kisha baada ya muda akanong’ona. Hatimaye alishindwa kustahimili, akaanza kulalamika kwa hadhara. Aliingiwa na mori akaipeana mikate yote iliyowasili kutoka Ulaya kwa majirani zake.

image

“Yaani mimi najinyima mengi maishani ili kumuelimisha mwanangu naye anaishia kunitunikia mikate? Hata haezi nitumia hata ndururu? Hana asante, huyo hata sio mototo wangu tena!” Mama huyo alifoka. Alizidi kuiipeana mikate yote kwa majirani, waliyoiparamia mithili ya mototo mchanga anayenyonya baada ya kulikosa titi la mamake mchana kutwa.
Siku moja Nzighe akabahatika kupewa likizo na waajiri wake, akaamua kusafiri hadi Madongoporomoka. Alipowadia alishanga kuiiona nyumba yao ingali katika shimo la umaskini lisilo na a wala be. Alipigwa na mshangao wakati mamake alimpa kisogo, akakataa katakata kumuamkua.
“Una nini mama?” Nzighe aliuliza. “Hatujaonana kwa mwongo mmoja nami nakuamkua na unakaa kimya? Kwani hujafurahia kuniona?”
Ndipo kichaa kilimpata nina. Aliruka kwa hasira kama mkizi na kumzaba kofi mwanaye. “Mkono birika wewe hata huna shukrani!” Alifoka kama joka. “Miaka kumi umefanya kazi Ulaya ndipo ushinde ukimtumia mamako mikate kila wiki? Ondoka machoni mwangu, baradhuli wewe! Sitaki kuwahi kukuona maishani mwangu, mende mkrofi wewe!”
Kusikia mamake akimfokea kulimvunja sana moyo Nzighe. Tufe la simanzi lilimkaba akaanza kulia shake. Alipanua mdomo kutaka kutamka neno ambalo lilipotelea mdomoni na kumuacha domo wazi ungedhani mtu mwenye mafua. Aliporejelewa na uwezo wa kusema, alimweleza mamake haya: “Mimi sio mkono birika mama. Sheria za kule Ulaya kwa sasa hazimkubalii yeyote kutuma pesa kutoka nchi hiyo. Kuna fashisti mmoja aliyemadarakani aliyepiga marufuku wageni kutuma pesa katika nchi zao za nyumbani, akidai kwamba pesa hizo zinafaa kuimarisha Ulaya. Ningekueleza haya kwenye barua lakini singeweza, kwani barua zote zitokazo nje ya nchi huwa zinasomwa kwa kina na wapelelezi wa kule. Nilikua na njia moja pekee ya kukutumia pesa, na nilihakikisha ya kwamba kila wiki nilikutumia takriban pauni mia saba niliyoioka ndani ya mikate ili isijulikane na wapelelezi.”
Mamake kusikia vile alipigwa na butwaa akashindwa hata kusimama. Ufunuo huo ulimuingia moyoni kama mshale wa moto. Mama na mwanawe walikumbatiana sakafuni, wakalia kilio cha mbwa midomo juu. Hadithi yangu imeishia hapo.”
Babu alipotamatisha hadithi yake iliyokolea huzuni sote tulisikitika pamoja na wahusika hao. Binamu wangu Amina alishindwa kuyazuia machozi, yakatiririka tiriri usoni mwake. Kakangu Jomba ndiye aliyekua wa kwanza kuzungumza. “Babu, ulitueleza wiki iliyopita ya kwamba hadithi ya leo itatufafanulia kinaga ubaga jinsi uliweza kuhamia Milimani kutoka mtaa wa vibanda,” Alianza Jomba. “Mbona umetuhadithia hadithi ya Nzighe?”
Babu alijitahidi kusimama na bakora yake kisha akajibu, “Miaka mingi iliyopita niliishi Madongoporomoka. Nilikua jirani wa mamake Nzighe na kila alipoletewa mikate kutoka Ulaya, mama huyo alinipea mimi mikate hiyo.”

Tabaruku
Shukrani zimuendee mwandani wangu Precious Nisii aliyekua wa kwanza kunihadithia kisa hiki.

Sharing is Caring...

Lukorito Jones

Lukorito Jones is a columnist and correspondent with Kenya's leading newspaper, Daily Nation. He also dabbles in fiction works at times, hoping to be the next Stephen King. Sometimes he takes time out from writing to perfect his deer-dancing and goat-screaming skills.

3 Comments:

  1. hadithi nzuri sana kakangu. kongole!

Please leave a comment and you will live happily ever after!