“Afadhali nife badala ya kujiuzulu!”


“Afadhali nife badala ya kujiuzulu!” Maneno haya yalihifadhiwa katika kumbukumbu za Kenya mwakani 2008 yalipotamkwa kwa ujeuri na Amos Kimunya. Bwana Kimunya, aliyekuwa Waziri wa Fedha, alikuwa anawajibu waliomsuta ajiuzulu kwa ajili ya sakata ya hoteli ya Grand Regency.

Hivi leo, yaonekana kwamba maneno ya Kimunya yametiliwa maanani sana na watumishi wa umma. Ni nadra sana kwa viongozi wetu kujiuzulu pasi na mapambano makali. Hata kukiwa na ushahidi mkubwa dhidi ya viongozi hao, wao bado husisitiza ya kwamba hawabanduki kamwe! Kiburi hiki cha viongozi wetu ni cha mshindo kweli!

Serikali yetu imejawa na watu wanaopora mali ya umma kama vile nzige huvamia shamba la mahindi. Viongozi wao hao ni wapotovu wa maadili na mara kwa mara huwa yabainika wazi wazi kwamba kazi imewashinda. Lakini majina ya waliojiuzulu kwa hiari yanahesabika kwenye kiganja kimoja tu! Desturi ya kujiuzulu ni jambo geni humu nchini.

Butwaa ilitupiga sote pale Waziri wa Utalii, Bwana Najib Balala, aliwaambia waliodai ajiuzulu “Nendeni Jehanam!” Hii ni licha ya waziri huyo kusimamia uhamishaji wa vifaru uliosababisha visa vya vifaru 10. Ingawa Balala aliomba msamaha, matamshi yake ya kuwaamrisha Wakenya waelekee Jehanamu bado yanauma hadi kwenye ini.

Siku kadhaa zilizopita, msimamizi wa tume ya mashamba Profesa Muhammad Swazuri alikataa kata kata kujiuzulu kufuatia sakata ya shamba la Ruaraka. Swazuri alitufokea eti, “Ni waoga pekee ambao hujiuzulu”.

Katika nchi zilizofaulu kidemokrasia, mambo huwa tofauti mno. Mwanzoni mwa mwaka, waziri nchini Uingereza alijizulu kutoka serikalini baada ya kuchelewa kufika bungeni. Afisa huyo alijieleza kwamba kukosa kufika bungeni kwa wakati ufaao kulimtia aibu kubwa. Waziri Mkuu wa nchi hiyo baadaye alikataa ombi lake la kujiuzulu. Je, hapa Kenya twaweza kuwalazimisha maafisa wa serikali kujiuzulu kwa ajili ya kutotilia wakati maanani?

Kwa hamaki, Balala alitueleza kwamba yeye anawajibikia mtu mmoja tu—Rais Uhuru Kenyatta. Usemi huo ni wa kusikitikisha, kwani hivyo ndivyo serikali za udikteta huendeshwa. Kwenye serikali za kidemokrasia, wananchi ndio waajiri wa mawaziri na viongozi wote serikalini. Balala anahitaji kuelewa kinagaubaga kwamba yeye ni mtumishi wa Wanjiku, na sharti ayajibu maswali yote yatakayoulizwa na Wanjiku.

Nafahamu kwamba sio vyema kwa watu ambao hawajihitimu sana kimasomo kumpinga profesa aliyebobea, lakini leo nitakaidi desturi na kumkosoa Profesa Swazuri. Swazuri alifoka kwamba ni waoga tu ambao hujiuzulu. Kwa upande wangu, kujiuluzu kutoka ofisini kunaonyesha ujasiri usio na kifani. Hii ni kwa maana kwamba mtu anapojitolea kujiuzulu, inaonyesha mtu huyu anadhamini nchi yake kuliko vile anavyodhamini vita vya kibinafsi.

Hivi leo, Kenya inatahitaji wafanyikazi wa umma walio na ujasiri wa kutosha kiasi kwamba wanaweza kujing’atua madarakani pindi tu madai ya hulka potovu yanapotolewa dhidi yao. Viongozi wanastahili kujifunza kwamba hata kama sio wao waliotenda maovu ila ni wadogo wao, viongozi hao wanapaswa kuwajibika na kujitwika mzigo wa lalama.

Maisha ya kibinafsi ya viongozi wetu pia yafaa yachunguzwe. Hii itawawezesha wananchi kukagua hulka ya viongozi. Ikiwa kiongozi atapatikana na hatia kama kumjeruhi mkewe au kumdhalilisha bawabu, basi kiongozi huyo sharti ajiuzulu.

Tukiendelea na mwenendo kama huo, tutaanza kushuhudia visa ambapo viongozi wetu wanajiuzulu kila ambapo serikali inaendeleza sera zinazokinzana na maadili yao ya kibinafsi. Kwa mfano, pale Rais atakapotoa amri kwamba watetezi wa haki za kibinadamu watiwe mbaroni, mawaziri wanaopinga agizo potovu kama hilo wanafaa wajiuzulu.

Leo hii, viongozi wetu ni wapotovu wa nidhamu wasioweza kujitwika lawama hata ikibainika bayana kwamba wameshindwa na kazi. Ukiwa mzalendo na uwashauri kwa ukarimu eti wajiuzulu, viongozi hao hukumiminia matusi mithili ya chiriku mlaani aliyeyanywa maji ya chooni. Wananchi wamegeuzwa maskwota na viongozi sasa ndio wenye nchi; hawaambiliki, hawasemezeki. Ni jambo la kusikitisha mno.Jones Lukorito ni mwanahabari.

Lukorito Jones

Lukorito Jones is a columnist and correspondent with Kenya's leading newspaper, Daily Nation. He also dabbles in fiction works at times, hoping to be the next Stephen King. Sometimes he takes time out from writing to perfect his deer-dancing and goat-screaming skills.

Please leave a comment and you will live happily ever after!